Viongozi wa dini wasifu siku 90 za Rais Samia Suluhu Hassan

0
173

Baadhi ya viongozi wa dini wamesifu siku 90 za Rais Samia ambazo ameweza kutekeleza majukumu yake mbalimbali ikiwemo uendelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa hapa nchini.

Akiongoza ibada katika kanisa la Kiinjili la Kulutheri Tanzania KKKT usharika wa Kimara mchungaji Wilbroad Mastai amesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa imara na kuendeleza yale yaliyofanywa na watangulizi wake.

“Ndani ya siku hizi 90 tuna jambo la kumshukuru Mungu maana bado tunaitwa Tanzania, bado Kuna amani, bado uzinduzi wa miradi unaendelea hakuna paliposimama, hii inatufanya kumrudishia Mungu asante maana waliowaza na kusubiri yatokee kinyume na haya walikuwa wengi” amesisitiza Mastai

Pia Mchungaji Mastai ameomba watanzania kuendelea kuomba Mungu katika masuala mbalimbali ikiwepo ugonjwa wa Corona ili Mungu awaepushe kama walivyofanya tangu janga hili lilipoikumba dunia

Kwa upande wake mchungaji Joseph Maseghe amesema watanzania wanapaswa kuwaombea viongozi katika nafasi zao ili Tanzania iendelee kuwa na Amani.

Kanisa hilo limefanya ibada mahususi kwaajili ya kumshukuru Mungu kwa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kipindi hiki tangu aingie madarakani kuwa Rais wa Tanzania kwa kutimiza siku 90 za uongozi wake na kumuombea kuiongoza Tanzania kwa kipindi chote atakachoongoza.