Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema kazi ya kumwongoza mwanadamu ni yenye mapito mengi, hivyo kwa kipindi cha uhudumu Mwadhama Kardinali Pengo amekuwa kiongozi wa kupigiwa mfano.
Dkt. Mpango ameeleza kuwa katika kutambua mchango wa Kardinali Pengo serikali itaendelea kushirikiana bega kwa bega na viongozi wa dini katika kuijenga nchi yenye amani na mshikamano.
“Kardinali Pengo wa amewahudumia wananchi bila ubaguzi huku anapoazimisha Miaka 50 ya utumishi wake Viongozi wa Serikali Wana mengi ya kujifunza kutoka kwake ikiwa ni pamoja na uvumilivu na hekima katika kuwaongoza watu,” amesema Dkt. Mpango.
Katika ibada hiyo pia ametoa fedha tasilimu kutoka ofisi ya Rais ikiwa ni pamoja na cheti cha heshima kwa Kardinali Pengo kutambua mchango wake ndani ya kanisa na katika shughuli zingine za kijamii.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Thadaeus Ruwa’ichi amebainisha kuwa kanisa linajivunia kumpata kiongozi huyo ndani na kwamba kazi zake zitabaki kuwa alama isiyofutika ndani ya jimbo hilo.
Akiwashukuru viongozi mbalimbali wa kiserikali na waamini walioungana naye katika ibada hiyo ya kumshukuru Mungu kwa miaka 50 ya Upadre, Kardinali Pengo amesema anaamini ushirikiano alioupata kwa waamini na viongozi wa Serikali katika awamu zote za uongozi uliopita zimekuwa chachu ya maendeleo katika kanisa na jamii kwa ujumla kata nyanja mbalimbali.
Kardinali Pengo alikabidhiwa Jimbo Kuu la Dar es Salama mwaka 1992 likiwa na Parokia 20 na mpaka anastaafu kama Askofu Mkuu ameacha Jimbo hilo likiwa na Parokia 118.