Kamati yaridhishwa na elimu ya uvuvi haramu bwawa la Mtera

0
207

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imeridhishwa na elimu iliyotolewa kuhusu uvuvi haramu kwa wavuvi wa bwawa la Mtera.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dkt. Christine Ishengoma ameyasema hayo baada ya kamati kumaliza ziara yake kwenye kijiji cha Misisiri wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma na kijiji cha Mnadani wilaya ya Iringa, ambapo walizungumza na wavuvi na wananchi wa maeneo hayo.

Dkt. Ishengoma amesema, katika vijiji vyote walivyopita wamekuta wavuvi na wananchi kwa ujumla wanayo elimu kuhusu uvuvi haramu na wanashiriki katika kudhibiti kwa kukamata nyavu haramu na kuziteketeza.

Naye Katibu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah amesema kuwa wizara imekuwa ikitoa elimu kuhusu uvuvi haramu na madhara yake kwa wavuvi na wananchi wanaolizunguka bwawa la Mtera ambapo kwa sasa wananchi hao wamekuwa wakishirikiana na serikali kudhibiti na kuteketeza nyavu zisizofaa zilizokamtwa.

Dkt. Tamatamah amewaahidi wavuvi wa kijiji cha Miseseri, kuwaletea injini moja ya boti mwezi Julai, 2021 ambayo pamoja na shughuli za uvuvi itawasaidia katika kufanya doria za kudhibiti uvuvi haramu.

Wananchi katika vijiji vyote viwili wameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge na wizara kwa kuwatembele na kusikiliza matatizo waliyonayo na wanaomani kuwa matatizo yao yatatafutiwa ufumbuzi.