Serikali imeanza kutekeleza mikakati yenye lengo la kuweka mazingira mazuri kwa Wakulima kupata mikopo, kwa ajili ya kuendesha shughuli zao.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Bungeni jijini Dodoma na kuongeza kuwa, miongoni mwa mikakati hiyo ni kuanzisha dawati la kuwasaidia Wakulima kuandika andiko la kuomba mikopo katika mabenki.
Akijibu maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu, Waziri Mkuu Majaliwa ameziagiza halmashauri zote nchini kuwa na dawati maalum la kuwasaidia wakulima kuandika andiko la kuomba mikopo benki kwani kuna wakulima wengi ambao hawawezi kufanya hivyo.
Amesema tayari Serikali imeanzisha benki maalum ya kilimo ambayo kazi yake kubwa ni kuwasaidia Wakulima.
Waziri Mkuu Majaliwa alikuwa akijibu swali la Mbunge wa viti maalum Jackline Kahinja aliyetaka kufahamu Serikali ina mikakati gani kuhakisha sekta ya kilimo inakua na inamnufaisha mkulima pamja na Taifa.