Siku tatu za kishindo kikuu cha Rais, Mwanza

0
355

Juni 15, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alihitimisha ziara yake ya siku tatu mkoani Mwanza, ikiwa ni ziara yake ya kwanza mkoani humo tangu alipoapishwa kuwa Rais (Machi 19, 2021) kufuatia kifo cha Dkt. John Magufuli (Machi 17, 2021).

Katika ziara hiyo iliyokuwa na kishindo kikubwa na yenye maamuzi magumu kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa, Rais Samia amefanya mambo mbalimbali kuanzia kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi mbalimbali, kufungua jengo la Benki Kuu ya Tanzania hadi kuzungumza na Taifa kupitia vijana wa Mwanza.

Katika hali ya ujumla tunakusogezea mambo mbalimbali aliyoyafanya Rais Samia Suluhu Hassan tangu alipowasili mkoani Mwanza Juni 13 hadi alipoondoka Juni 15.

Siku ya kwanza alianza kwa kuzindua mtambo wa kusafisha dhahabu wa Kampuni ya Mwanza Precious Metals Refinery Limited uliogharimu shilingi bilioni 12.2. Pamoja na mambo mengine, mtambo huo utaongeza mapato ya Serikali kupitia mrabaha, tozo za ukaguzi na ushuru wa huduma na kutoa ajira za moja kwa moja 120 na zisizo za moja kwa moja 400.

Mtambo huo na mingine miwili iliyopo nchini ambayo ni matokeo ya mabadiliko ya sheria katika sekta ya madini imeongeza mapato ya madini kutoka shilingi bilioni 168 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 528 mwaka 2020. Pia utasaidia kuchochea shunguli za uchimbaji dhahabu na kuiwezesha Benki Kuu ya Tanzania kununua dhahabu na hivyo kuwezesha nchi kuwa na amana ya dhahabu kwa kiwango kikubwa.

Katika siku hiyo pia Rais alifungua jengo jipya la Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Tawi la Mwanza na kuipongeza benki kuu kwa mafanikio mbalimbali iliyoyapata ikiwa ni pamoja na kuimarisha uchumi.

Tawi la BOT mkoani Mwanza ni lilianzishwa mwaka 1980 na ni miongoni mwa matawi manne ya BOT nchini ambapo mengini ni Arusha, Mtwara na Mbeya. Tawi hilo linahudumia mikoa saba ya Kagera, Simiyu, Kigoma, Mwanza, Geita, Shinyanga na Mara.

Rais alitumia jukwaa hilo kuitaka BOT kufanya maandalizi ya matumizi ya safaru za kimtandao (blockchain/cryptocurrecy) kwani mabadiliko hayo ya kiteknolojia yanaweza kuikumba Tanzania, hivyo ni vyema wakati yanafika nchini yasiikute nchi haijajiandaa.

Juni 14 (siku ya pili ya ziara) Rais alianza kwa kukagua ujenzi wa Daraja la JPM (Kigongo – Busisi) lenye urefu wa kilomita 3.2 ambalo litagharimu shilingi bilioni 716 na litakapokamilika litafungua fursa zaidi za kiuchumi.

Rais Samia Suluhu Hassan alisema Serikali imepeleka wakaguzi maalum kwa ajili ya kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali za kifedha zinazoikabili Halmashauri ya Sengerema.

Baada ya hapo Rais alizindua mradi wa maji katika eneo la Misungwi ambao unaohusisha miji ya Magu na Lamadi, umegharimu shilingi bilioni 45. 57 na utawahudumia wananchi zaidi ya 64,000.

Rais alitumia jukwaa hilo kuiagiza Wizara ya Maji kuhakikisha miradi yote ya maji inatekelezwa kwa wakati ili kufikia lengo la Serikali la kuwaondolea wananchi adha ya upatikanaji wa maji.

Katika siku ya pili pia alipata fursa ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya Mwanza – Isaka yenye urefu wa kilometa 341, utakaogharimu shilingi trilioni 3.06. Alisema mradi huo utaongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kwa kusafirisha kwa haraka na kwa kiwango kikubwa cha mizigo na watu tofauti na ilivyo sasa.

Siku ya mwisho ya ziara yake mkoani Mwanza alianza kwa kuzungumza na vijana ambapo aliwataka kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazopatikana katika miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali na fursa za uchumi mtandao.

Baadhi ya maagizo aliyotoa ni pamoja na Chama cha Mapinduzi (CCM) kukarabati viwanja inavyomiliki ili vijana waweze kuvitumia, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kujenga shule za michezo ( Sports Academy) katika mikoa na kujenga kumbi za kisasa za burudani na michezo (Sports Arena) ambazo wasanii watazitumia katika majira yote ya mwaka.

Katika hali ambayo haikutarajiwa Rais alitengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Bakari Msulwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba kwa kushindwa kusimamia Wafanyabiashara wadogo ambapo alieleza kukerwa na kitendo cha askari mgambo kutumia nguvu kuwafukuza wamchinga kutoka eneo walilokuwepo.

Rais alimaliza ziara yake kwa kuzindua Chelezo ambayo imekamilika kujengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 36.4. Chelezo hiyo kwa sasa inatumika kutengeneza Meli mpya ya MV. Mwanza pia kitatumika kutengeneza na kukarabati meli nyingine hapa nchini na hata kutoka nje ya nchi.

Rais Samia pia amezindua meli mbili za New Butiama na New Victoria ambazo zimefanyiwa ukarabati mkubwa na kwa sasa zinatoa huduma kama awali kwa kusafiri kati ya Mwanza na Bukoba na Nansio Ukerewe.

Pia alishuhudia utiaji saini wa mikataba mitano ya ujenzi na ukarabati wa Meli ambazo baadhi yake zitatumika kutoa huduma katika Ziwa Tanganyika na bahari ya Hindi, zitakazogharimu zaidi ya shilingi bilioni 438.

Baada ya kumaliza ziara hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan amerejea jijini Dar es Salaam kuendelea na majukumu mengine.