Watu 11 wamethibitika kufa katika jimbo la Baidoa nchini Somalia kufuatia ghasia zilizozuka baada ya kukamatwa kwa Kamanda wa zamani wa Wanamgambo wa Al-Shabab, – Mukhtar Robow.
Miongozi mwa watu waliokufa katika ghasia hizo ni Mbunge wa jimbo hilo la Baidoa.
Mbali na vifo, ghasia hizo pia zimesababisha hasara ya mali ikiwa ni pamoja na magari kuchomwa moto na kuharibiwa kwa majengo mbalimbali.
Miezi miwili iliyopita, serikali ya Somalia ilimzuia Robow kushiriki katika kinyang’anyiro cha Ubunge katika jimbo la Baidoa lakini Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo ilimpa ruhusu ya kushiriki katika kinyang’anyiro hicho.
Kwa muda mrefu, serikali ya Somalia imekua ikimshutumu Robow na kusema kuwa ni tishio kubwa kwa usalama wa Taifa hilo.
Kamanda huyo wa zamani wa Wanamgambo wa Al-Shabab wa nchini Somalia, – Mukhtar Robow ana umri wa miaka 46 na alipata mafunzo yake ya kigaidi nchini Afghanistan, mafunzo yaliyomuwezesha kuwa miongoni mwa waanzilishi wa mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda.