Wahalifu watumiwa salamu

0
205

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI) Camilius Wambura, amesema Jeshi la Polisi Nchini halitamvumilia mtu yeyote atakayeendelea  kujihusisha na vitendo vya uhalifu hasa wakati huu ambao jeshi hilo linaendelea na operesheni kali ya kupambana na vitendo hivyo.

DCI Wambura ameyasema hayo jijini Dodoma katika kikao kazi kilichowashirikisha Maofisa wa Makao Makuu ya Upelelezi na Wakuu wa Upelelezi wa mikoa nchini, kwa lengo la kupanga mikakati ya kupambana na uhalifu  pamoja na kutathmini hali ya uhalifu nchini.

Amemtaka mtu yeyote anayejihusisha na vitendo vya uhalifu kuacha mara moja, kwa kuwa hivi sasa operesheni inaendelea nchi nzima ya kuwasaka.

DCI Wambura amesema kuwa, katika kuhakikisha operesheni hiyo inafanikiwa, ameona ni bora kukutana na Wakuu hao wa Upelelezi kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar ili kwa pamoja waweke mikakati ambayo italenga kutokomeza uhalifu hapa nchini.

“Wito wangu kwa wahalifu ni bora   watafute kazi nyingine ya kufanya kwa kuwa hatuna huruma kwa watu hao, na Wananchi waendelee kutupatia taarifa zao ili tuhakikishe nchi yetu inaendelea kuwa salama.“ amesema DCI Wambura.