Serikali yahimiza shule za msingi zifundishie elimu ya watu wazima

0
199

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewakumbusha wadau wa elimu nchini kutumia madarasa ya shule za msingi kutolea elimu ya watu wazima ikiwa ni juhudi za kutoa elimu kwa watu wengi hapa nchini

Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia Profesa Joyce Ndalichako ametoa rai hiyo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Miaka 50 ya Elimu Watu Wazima Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Ndalichako amewataka wadau wa Elimu kushirikiana na serikali kuboresha utoaji wa elimu ya watu wazima ili kuwarahisishia Watanzania wanaotaka kupata elimu hiyo.

“Nikumbushe tu wadau wanaopenda kutoa elimu kwa watu wazima, serikali ilisharuhusu kutumia shule za msingi kutoa elimu kwa watu wazima hivyo wajitokeze kuanzisha programu hizo na sisi tutashirikiana nao katika kutoa elimu hiyo ili kuwasaidia Watanzania,” amesisitiza Prof. Ndalichako

Katika kujenga uelewa wa elimu ya watu wazima Waziri Ndalichako amesema Serikali ina mpango wa kushirikiana na vyombo vya habari kutoa hamasa kwa watu.

“Kazi za kutoa elimu ya watu wazima zinafanyika ila naona hakuna uhamasishaji, hivyo tunakusudia kutumia vyombo vya habari kutoa hamasa watu wajipatie elimu hiyo,” ameeleza Ndalichako

Kongamano la Kimataifa la miaka 50 ya elimu watu wazima la siku tatu limefunguliwa leo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kaulimbiu ni, Elimu ya Watu Wazima kwa Maendeleo Endelevu.