Wanafunzi kulamba bilioni 500 mwaka 2021/2022

0
156

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza kuwa dirisha la maombi ya mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya juu kwa mwaka 2021/2022 linatarajia kufunguliwa Julai Mosi mwaka huu.

Akizungumza mkoani Dar es salaam wakati wa hafla ya utiaji saini wa hati ya makubaliano baina ya HESLB na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amesema kabla ya kufunguliwa kwa dirisha la maombi, tarehe 25 mwezi huu HESLB itatoa mwongozo wa uombaji mikopo.

Badru amesema HESLB imekamilisha maandalizi yote kwa ajili ya msimu mpya wa masomo wa mwaka 2021/2022, na kuwataka Wanafunzi wahitaji kutumia muda uliopo kwa ajili ya kukamilisha taratibu mbalimbali za uombaji mikopo.

“Tunawasihi wanafunzi kusoma kwa makini mwongozo wa uombaji mikopo utakaopatikana katika tovuti yetu ambayo ni www.heslb.go.tz ambao utachapishwa katika lugha ya kiingereza na Kiswahili, kabla ya kufungua dirisha la maombi Mwanafunzi anapaswa kusoma mwongozo huo,” amesema Badru.

Kuhusu bajeti ya mikopo, Badru amesema katika mwaka wa masomo 2021/2022 Serikali imetenga shilingi bilioni 500 kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu inayotarajia kunufaisha jumla ya Wanafunzi laki moja na sitini.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA Emmy Hudson amesema Wakala huo umekamilisha hatua mbalimbali za kuwawezesha Wanafunzi wahitaji, ikiwemo kutoa mwongozo wa uhakiki wa vyeti  vya kuzaliwa ambavyo ni moja ya nyaraka muhimu zinazohitaji wakati wa kuomba mikopo.