Watanzania washauriwa kuongeza ulaji wa nyama

0
201

Pamoja na kuwa na mifugo mingi, Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo Wananchi wake hawali nyama kwa wingi kama inavyoshauriwa kiafya.

Akizungumza katika mahojiano na Mwandishi wa TBC mkoani Dar es salaam, Msajili wa Bodi ya Nyama nchini Dkt. Daniel Mushi amesema kuwa takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2020/2021Tanzania imezalisha zaidi ya tani laki saba za nyama ikiwa ni wastani wa kilo 15 kwa kila Mtanzania kwa mwaka.

Dkt. Mushi ameongeza kuwa Shirika la Afya Duniani (WHO) limekuwa likishauri kila mtu kula kilo 50 za nyama kwa mwaka, kiasi anbacho kwa Tanzania haijafikia hata kwa nusu.

Aidha, Dkt. Mushi ameeleza kuwa nyama nyekundu ni muhimu kwa afya ya binadamu, ingawa si nzuri sana kula zaidi ya gramu 70 kwa siku, kutokana na kuwa na madini mengi ya chuma.

Akizungumzia changamoto mbalimbali zinazoikabili Bodi ya Nyama Nchini, Dkt. Mushi ametaja miongoni mwa changamoto hizo kuwa ni kutokuwa na takwimu sahihi za ulaji wa nyama kwa kuwa bado watu wengi wamekuwa wakichinja mifugo majumbani mwao.