Aliyehifadhi viatu vya Mzee Mandela Tanzania afariki dunia

0
234

Vicky Nsilo Swai, aliyekuwa mke wa Mwanasiasa mkongwe, mpigania uhuru na waziri wa zamani wa Tanzania, Asanterabi Nsilo Swai, amefariki dunia nyumbani kwake Soweto mkoani Kilimanjaro.

Enzi za uhai wake, Vicky Nsilo Swai aliwahi kuhifadhi nyumbani kwake viatu vya mpigania uhuru na Rais wa kwanza wa Afrika Kusini mwenye asili ya Afrika, Hayati Mzee Nelson Mandela, ambavyo aliviacha nyumbani kwa Mzee Nsilo Swai alipoingia Tanzania kwa mara ya kwanza mwaka 1962 akitokea Afrika Kusini ili kuanza harakati za ukombozi.

Mwezi Desemba 2013, Vicky Nsilo Swai alikuwa ni miongoni mwa Watanzania wachache walioongozwa na Dkt. Jakaya Kikwete wakati huo akiwa Rais wa Tanzania, kushiriki kwenye mazishi ya Mzee Mandela yaliyofanyika katika Kijiji cha Qunu nchini Afrika Kusini.

Vicky aliwahi kuwa Mwenyekiti wa CCM mkoani Kilimanjaro kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2002 hadi mwaka 2012.

Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amesema kuwa katika kipindi chake cha uongozi Vicky aliwakutanisha wanasiasa wengi waliokuwa wanataka kuzikomboa nchi zao, na pia alikuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo wa Uenyekiti wa CCM kwa mkoa huo.