Mwongozo wa uwekezaji Mara wazinduliwa

0
204

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza Viongozi wa mkoa wa Mara na Watendaji katika sekta ya utalii mkoani humo, kuweka mikakati ya kuitangaza mbuga ya Serengeti ili kuvutia zaidi watalii na kuitambulisha mbuga hiyo kuwa iko mkoani humo.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo mjini Musoma, wakati akizindua mwongozo wa Uwekezaji wa mkoa wa Mara.

Amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inaboresha mazingira ya uwekezaji na biashara, ili kuvutia uwekezaji utakaoinua uchumi wa nchi na watu, na mwongozo huo ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuvutia uwekezaji na kuimarisha biashara.
 
Waziri Mkuu Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwaagiza Viongozi wa mkoa wa Mara kuhakikisha watendaji, wataalam na wananchi wanakuwa nyenzo ya kurahisisha kazi ya kuvutia uwekezaji.
 
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa hakikisha watendaji wote wa mkoa wanausoma na kuuelewa ipasavyo mwongozo huu, hakikisha watendaji wako wanatekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uaminifu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
 
Waziri Mkuu amesema mkoa wa Mara una fursa nyingi za uwekezaji ambazo endapo zitatumika vema, zinaweza kuipaisha nchi kimaendeleo.
 
Ametaja miongoni mwa maeneo ambayo mkoa wa Mara unaweza kunufaika zaidi kwenye uwekezaji kutokana na fursa zilizopo ni kilimo, mifugo na uvuvi.