Waziri Mkuu awasimamisha kazi watendaji wa wizara ya fedha

0
468
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Wakuu wa Mikoa , Makatibu Tawala wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Mikoa kwa njia ya video akiwa ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma, Machi 21, 2020.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi Mkaguzi Mkuu, Mkaguzi Msaidizi pamoja na baadhi ya watendaji wa Wizara ya Fedha na Mipango ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma zinazowakabili.

Akizungumza katika Kikao Kazi na Waziri wa Fedha na Mipango, Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Kamishna wa Polisi, Salum Rashid Hamdun kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma hizo na ikithibitika kwamba tuhuma si za kweli wahusika watarejeshwa kazini.

Waziri Mkuu amezitaja baadhi ya tuhuma hizo kuwa ni malipo yaliyofanyika Machi 31 mwaka huu kupitia vocha 30 ya shilingi milioni 251 yakielezwa kuwa ni malipo maalum bila kutaja kazi hiyo maalum ni kazi gani na nani aliifanya hiyo kazi.

Amesema siku hiyo hiyo ya Machi 31 pia zililipwa shilingi milioni 198.8 kwa madai kuwa ni posho ya honoraria.

Majaliwa amesema Aprili 8 mwaka huu watumushi 27 wa wizara hiyo walilipwa shilingi milioni 44.5 zikiwa ni posho ya kazi maalum ya wiki nne. Pia Aprili 13 mwaka huu zililipwa shilingi milioni 155.2 kwa watumishi 68 ikiwa ni posho ya ya kazi maalum ya wiki tatu.

Aidha, Aprili 30 mwaka huu zililipwa shilingi milioni 43.9 kwa ajili ya kuandaa mpango wa kuhifadhi mazingira na siku hiyo hiyo zililipwa shilingi milioni 14.4 kwa ajili ya siku ya wanawake. Fedha nyingine shilingi milioni 43 zililipwa siku hiyo na kufanya jumla ya malipo yaliyolipwa siku hiyo kuwa shilingi milioni 101.8.

Amesema kuwa, Mei 1 asubuhi mwaka huu zililipwa shilingi milioni 184.1 na mchana zililipwa shilingi milioni 264 zikiwa ni malipo ya kazi maalum. “Sisi tulikuwa Mwanza tunasherehekea siku ya wafanyakazi duniani nyinyi hapa ndani mnalipana posho.”

Ameongeza kuwa Mei 3 mwaka huu zililipwa shilingi milioni 146.5 kwa watumishi 125 zikiwa ni malipo ya kuandaa Mpango Kazi wa Manunuzi kazi ambayo ni sehemu ya majukumu yao ya kila siku. Tarehe hiyohiyo zililipwa shilingi milioni 171.2 kwa ajili ya kuandaa nyaraka za Bunge.

Aidha, Waziri Mkuu amesema shilingi milioni 155 zililipwa kwa baadhi ya watumishi zikiwa ni posho ya kuandaa miongozo wakazi. ” Yaani hii kazi ya ukaguzi imelipwa kwenye maeneo manne, huu ni utaratibu wa wa wapi? Mnazidi kutupunguzia imani, na sijaongelea eneo la kuhamisha mafungu na utaratibu kuhamisha fedha kisha mnakwenda kuzichukuwa huko mlikozihamishia.”

Aidha, Waziri Mkuu amewataka watendaji wa Wizara hiyo kujenga uaminifu kwa wanaokusanya mapato kwa kufanya kazi kwa uaminifu na ametahadharisha kuwa watakaoendekea kucheza na pesa za umma hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

Wakati huo huo, amewapongeza watendaji wengine wa wizara hiyo ambao wameendelea kufanya kazi kwa weledi.