Ore wa Mahakama ya Afrika amuaga Rais

0
194

Rais Samia Suluhu Hassan leo amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Sylvain Ore ambaye anamaliza muda wake mwisho wa mwezi huu.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam, Rais Samia Suluhu Hassan ameipongeza Mahakama hiyo ambayo makao yake makuu yapo jijini Arusha kwa kazi inazozifanya na amemhakikishia Ore kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano ikiwa ni pamoja na kushughulikia changamoto mbalimbali kwa kuwa inatambua umuhimu wa majukumu yake.

Aidha, Rais Samia Suluhu Hassan amempongeza Ore kwa utumishi wake wa vipindi viwili vya Urais wa Mahakama hiyo ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu
na amemuomba kuendelea kuwa Balozi mwema wa Tanzania.

Kuhusu Tanzania kufuta tamko la kuruhusu taasisi zisizo za kiserikali na watu binafsi kupeleka mashauri yao moja kwa moja katika Mahakama hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania italiangalia jambo hilo lakini kwa sasa msimamo haujabadilika.

Kwa upande wake, Rais huyo wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Sylvain Ore amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano ambao Mahakama hiyo imeupata kwa kipindi chote cha uongozi wake, na amemhakikishia kuwa Tanzania ni sehemu sahihi ya Mahakama hiyo kuwepo kutokana na uwepo wa amani, utulivu na mandhari ya kuvutia.

Ore ambaye ametumia fursa hiyo kumuaga Rais amebainisha kuwa, katika kipindi cha uongozi wake Mahakama hiyo imeendelea kutekeleza majukumu yake vizuri na kufikia matarajio ya Bara la Afrika.