Rugemalira na wenzake hali bado tete

0
200

Na Emmanuel Samuel

Upande wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mshtakiwa James Rugemalira na wenzake wawili, umeiomba mahakama ya hakimu mkazi Kisutu iliyopo mkoani Dar es salaam kutoa mwongozo ama amri inayofaa juu ya kesi hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na wakili wa James Rugemalira, -John Chuma mbele ya Hakimu Mkuu wa mahakama hiyo Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.

Akiwasilisha hoja zake Wakili Chuma amedai kuwa mshtakiwa James Rugemalira ambaye hakuwepo mahakamani wakati kesi hiyo ilipotajwa, ameiandikia mahakama hiyo maelezo mafupi yanayohusu matukio ya nyuma juu ya shauri hilo, hivyo kuomba mahakama kutoa mwongozo ama amri inayoona inafaa juu ya muenendo wa kesi hiyo.

Baada ya kusikiliza hoja hiyo, Hakimu Shaidi amedai kuwa mahakama iliishatoa mwongozo juu ya kesi hiyo, hivyo haoni sababu ya kutoa mwongozo mwingine.

Aidha upande wa Jamhuri unaowasilishwa na Wakili Mwandamizi Wankyo Simon umedai kuwa, mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo Habinda Seth bado anaendelea na mazungumzo na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka juu ya kumaliza shauri lake na hivyo kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine na kwamba upepelezi wake haujakamilika.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 3 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.