Rais Samia Suluhu Hassan : Msitumie makosa kama kitega uchumi

0
291

Rais Samia Suluhu Hassan ameliagiza Jeshi la Polisi nchini kujielekeza zaidi katika kutoa elimu ya usalama barabarani kwa Wananchi,  na si kuwa na sheria za kuadhibu zinazotumika kama njia za kujipatia mapato.

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo katika Chuo Cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam, baada ya kuzindua kiwanda cha ushonaji cha Jeshi la polisi.

Amesema Jeshi la Polisi nchini limekuwa likitoa elimu ya usalama barabarani kupitia vipindi mbalimbali kikiwemo kile cha UBU kinachotangazwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), lakini liongeze kasi katika kutoa elimu hiyo.

Kuhusu hali ya usalama nchini, Rais Samia Suluhu Hassan amempongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Simon Sirro kwa kutekeleza agizo lake alilolitoa hivi karibuni la kutaka kudhibitiwa kwa vitendo vya uhalifu ambavyo vimekuwa vikijitokeza katika maeneo mbalimbali nchini.

Hata hivyo, ametaka kudhibitiwa kwa  wale wote wanaolijaribu Jeshi la Polisi kwa kuendeleza vitendo vya uhalifu.

Rais Samia Suluhu Hassan ameongeza kuwa kuanzia sasa miongoni mwa vigezo atakavyotumia katika kuwapandisha vyeo Makamanda wa polisi  ni namna ambavyo wamekuwa wakikabiliana na vitendo vya uhalifu katika maeneo yao.