Watu wawili waliotoka gerezani hivi karibuni kwa msamaha wa Rais wameuawa baada ya kukamatwa wakidaiwa kuiba vitu mbalimbali huko Kwa Mathias wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Pwani, -Wankyo Nyigesa amesema watu hao wameuawa kwa kupigwa na mawe, mapanga na fimbo na Wananchi wenye hasira waliowatuhumu kuhusika na wizi huo.
Amewataja watu hao kuwa ni Ramadhani Mohamed maarufu kwa jina la Seven au Ali mwenye umri wa miaka 28 mkazi wa Kwa Mathias na Idd Hamisi maarufu kama Chuga mwenye umri wa miaka 30 mkazi wa mtaa Jamaica wilayani Kibaha, ambao wote walikuwa wamerudi uraiani hivi karibuni kwa msamaha wa Rais.
Watu hao walifungwa kwa makosa ya wizi katika kesi ya jinai namba 273/2020 na 260/2020, na walipata msamaha huo wa Rais Aprili 12 mwaka huu kutoka katika gereza la Mkuza mjini Kibaha.
Kufuatia tukio hilo, Kamanda Nyigesa amewashauri Wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi, na badala yake watoe taarifa polisi linapotokea tukio la wizi kwenye maeneo yao ili watuhumiwa wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.