Na,Emmanuel Samwel,TBC
Mwanasheria wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), ambaye pia ni mshitakiwa katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wa kampuni hiyo, Joseph Makandege, ameondoa rasmi maombi yake ya kufanya majadiliano na serikali ili kuimaliza kesi inayowakabili
Hatua hiyo imekuja baada ya kupita siku 45 zilizotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mshtakiwa huyo na wenzake kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini( DPP.) ili kumaliza kesi inayowakabili.
Makandege kupitia wakili wake, Alex Balomi ameieleza Mahakama hiyo leo Mei 6, 2021, kuwa wameamua kujitoa katika mashauriano na DPP baada ya kukosa ushirikiano kutoka katika ofisi hiyo ya mashitaka hapa nchini.
Makandege na wenzake Harbinder Seth na James Rugemalira, walipewa nafasi ya kuzungumza na DPP ili kuangalia namna wanavyoweza kumaliza shauri hilo nje ya Mahakama.
Akijibu hoja za wakili wa watuhumiwa, wakili wa Serikali Faraja Nguka ameieleza Mahakama hiyo kuwa majadiliano ya kumaliza kesi hiyo bado yanaendelea katika ofisi ya DPP.
Baada ya Hakimu anayesikiliza shauri hilo Huruma Shaidi kusikiliza hoja za pande zote mbili, aakatoa maelekezo kwa ofisi ya DPP kutumia Mamlaka aliyonayo kutekeleza wajibu wake.
Mnamo Februari 25, 2021, mahakama hiyo iliamuru majadiliano ya kukiri mashtaka yaliyowasilishwa kwa DPP dhidi ya Seth na Makandege, yasikilizwe ndani ya siku 30, kuanzia siku hiyo.
Shauri hilo limeahirishwa hadi Mei 20, 2021 na litaletwa kwa ajili ya kutajwa.