Bashungwa aagiza kulindwa kazi za Wasanii

0
720

 
Waziri ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa ameliagiza Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) na Bodi ya Filamu Tanzania (TFB) kufanya uhakiki wa kazi za sanaa kwa utaratibu ambao haukwamishi kazi za wasanii nchini.

Waziri Bashungwa ametoa agizo hilo jijini Arusha na kuongeza kuwa uhakiki unaofanywa na taasisi hizo lengo lake ni kulinda maadili ya Mtanzania bila kuathiri ubunifu wa wasanii, maendeleo ya sanaa nchini na kuhakikisha haudumazi ukuaji wa ajira.

 “Kwa upande wa filamu uhakiki unasaidia kujua maudhui yaliyopo kwenye filamu husika ili kuamua ipangiwe daraja gani na unasaidia kuepusha maudhui mabaya ya kuharibu maadili ya jamii yetu, yadhibitiwe kabla ya kufika kwa mtazamaji/msikilizaji,” amesema Waziri Bashungwa.

Ameongeza kuwa wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inaendelea kupokea maoni na kukutana na Wadau ikiwa ni sehemu ya namna ya kuboresha chambuzi na hoja zilizowasilishwa ambazo zitasaidia kuziunganisha BASATA, COSOTA na TFB ili kuleta tija na kusimamia kazi za sanaa na wasanii nchini.

Waziri Bashungwa amewasisitiza wadau hao wa Sanaa ambao hawajawasilisha maoni yao kuendelea kuyawasilisha, kwani yatasaidia kuwa na sheria na kanuni zinazosimamia maudhui ya kazi za sanaa kupitia taasisi hizo ili yasiende kinyume na mila, desturi na utamaduni wa Mtanzania.