Vijana wa kujitolea JKT warejeshwa katika mafunzo

0
240

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limewarejesha katika mafunzo vijana waliochaguliwa kujiunga na jeshi hilo kwa kujitolea kwa mwaka 2020/202, baada ya kurejeshwa nyumbani mwezi Februari mwaka huu.
 
Kaimu Mkuu wa Utawala Tawi la JKT, Kanali Hassan Mabena amesema kuwa vijana hao wanatakiwa kuripoti  katika kambi  walizokuwa wamepangiwa awali kuanzia Mei 7 hadi 14 mwaka huu.
 
Amefafanua kuwa vijana waliorejeshwa ni wale wenye elimu ya darasa la saba na kidato cha nne.
 
“Vijana wenye elimu ya kidato cha sita, ngazi ya cheti, stashahada, shahada na wale wenye taaluma ya Uhandisi wataendelea kusubiri majumbani hadi hapo utaratibu mwingine utakapotangazwa,” amesisitiza Kanali Mabena.
 
Jeshi la Kujenga Taifa limekuwa likiendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana kwa kuwapa stadi za maisha ikiwa ni pamoja na uzalishaji mali, uzalendo, kilimo, ufugaji na kushiriki katika ujenzi wa Taifa.