Mkuu wa wilaya ya Arusha,- Kenani Kihongosi amefanya ziara ya kutembelea hospitali ya wilaya ya Arusha iliyojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya kuwahudumia Wakazi wa jiji la Arusha.
Wakati wa ziara hiyo, Kihongosi ameridhishwa na ujenzi wa majengo mbalimbali hospitalini hapo, likiwemo lile la mama na mtoto ambalo amesema limejengwa kwa ufanisi mkubwa.
Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha huduma za afya ndani ya jiji la Arusha pamoja na kupeleka vifaa vya kisasa vya kutolea huduma katika hospitali hiyo.
Amewaomba Wakazi wa jiji la Arusha na Watanzania wote kuendelea kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan ili azidi kuchapa kazi na Taifa liendelee kusonga mbele.
Kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa hospitali hiyo ya wilaya ya Arusha, Kihongosi pia amempongeza Mkurugenzi wa jiji la Arusha Dkt. John Pima kwa kutumia mapato ya ndani katika ujenzi huo na Mganga Mkuu wa wilaya pamoja na wataalamu wote wa afya kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwahudumia Wananchi.
Mkuu huyo wa wilaya ya Arusha amewataka Watumishi wote wa wilaya hiyo kuwa na umoja na mshikamano na wawe wazalendo kwa nchi yao.