Maandamano yapigwa marufuku Chad

0
209

Polisi nchini Chad wamezuia maandamano katika mji mkuu wa nchi hiyo N’Djamena, ambapo Wananchi wanaandamana kupinga hatua ya jeshi la nchi hiyo kuchukua madaraka.

Polisi hao wametumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji ambao wamekuwa wakichoma moto matairi katika mitaa mbalimbali ya mji wa N’Djamena, na miji mingine ya jirani.

Ghasia zimezuka katika maeneo mbalimbali nchini Chad, saa chache baada ya jeshi la nchi hiyo kutangaza kuzuia maandamano yote nchini humo.

Tangazo hilo limetolewa ikiwa imepita wiki moja tangu Jeshi la Chad kuchukua jukumu la kuiongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miezi 18 kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais Mteule wa Taifa hilo Idriss Déby.

Idriss Déby alifariki dunia baada ya kupata majeraha wakati wa mapambano baina ya vikosi vya Serikali vya nchi hiyo na Waasi.

Kwa sasa Chad inaongozwa na Baraza la Kijeshhi kwa kipindi hicho cha miezi 18 mpaka hapo utakapofanyika uchaguzi wa Rais.

Baraza hilo linaongozwa na mtoto wa kiume wa Idriss Déby, – Jenerali Mahamat Idriss Déby Kaka.