BAKITA yatakiwa kuongeza nguvu ya kutafsiri miswada ya sheria

0
313

Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limeagizwa kuongeza nguvu katika kutafsiri miswada ya sheria mbalimbali na kanuni zake, ili kuwawezesha Wananchi kuzifahamu kwa lugha ya kiswahili.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Paulin Gekul ametoa agizo hilo mkoani Dar es salaam, alipokuwa akizungumza na uongozi wa BAKITA.

Amesema Wananchi wengi wanashindwa kuzielewa sheria na kanuni zake kutokana na kuandikwa kwa lugha ya Kiingereza, ambayo haieleweki kwa watu wengi.

Aidha, Naibu Waziri Gekul ameitaka BAKITA kuangalia namna ya kushirikiana na Balozi mbalimbali za Tanzania kuanzisha vituo vya kufundishia lugha ya kiswahili katika nchi mbalimbali Barani Afrika, kwa lengo la kukuza lugha hiyo.

Ameongeza kuwa BAKITA inapaswa kumalizia istilahi ya kiswahili itakayotumika kufundishia somo la historia ya Taifa.

Mpaka sasa BAKITA ina vituo 14 vya ndani vya kufundishia lugha ya kiswahili, na kituo kimoja cha kufundishia lugha hiyo kilichopo nchini Afrika Kusini.