Morogoro mbioni kumaliza migogoro ya ardhi

0
174
Mgeni rasmi Mhandisi Emmanuel Kalobelo, Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro akipewa maelezo ya vifaa vya upimaji vinavyotumiwa na wanafunzi katika mafunzo kwa vitendo na mmoja wa wahitimu kutoka Chuo cha Ardhi Morogoro kabla sherehe za mahafali ya 39 hazijaanza.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Kalobelo amemwagiza Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro kuandika barua kwenda halmashauri zote za Mkoa huo kuona jinsi gani wanaweza kuwatumia wataalam kutoka chuoni hapo kumaliza migogoro ya ardhi inayosababishwa na ujenzi holela na kugombania mipaka ya maeneo.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi katika mahafali ya Chuo cha Ardhi Morogoro amesema, ‘‘ni aibu kwa Mkoa wa Morogoro kuendelea kuteseka na migogoro ya ardhi wakati chuo kinachozalisha watalaam wa kupanga na kupima kipo hapa hapa. Naagiza kabla mwaka huu haujaisha Halmashauri zote za mkoa wa Morogoro ziwe na mpango mkakati kuona jinsi gani ya kushirikiana na Chuo cha Ardhi Morogoro kuhakikisha kila kipande cha ardhi kinapangwa, kupimwa na kumilikishwa”, amesema Mhandisi Emmanuel.

Mbali na kuzalisha wataalam wa kupanga na kupima, chuo hicho kimekuwa kikishiriki kutoa huduma ya ushauri wa kitaalamu na kufanya miradi ya urasimishaji ambayo hadi sasa inatekelezwa katika mikoa ya Dar es salaam, Arusha, Morogoro, Mtwara, Kilimanjaro na Iringa.