Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mwanza imemkamata aliyekuwa Mhasibu wa Mamlaka ya Bandari Kigoma, – Madaraka Robert ambaye anatuhumiwa kwa makosa ya rushwa, uhujumu uchumi na ukwepaji kodi ya zaidi ya shilingi milioni 150.
Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Mwanza, – Frank Mkilanya amesema kuwa Madaraka ambaye ni mmoja wa watuhumiwa waliokuwa watumishi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania mkoa wa Kigoma, amekamatwa akiwa mafichoni katika eneo la Nyasaka wilaya ya Ilemela mkoani humo.
Amesema Madaraka alikuwa akitafutwa na TAKUKURU tangu mwezi Agosti mwaka 2020, ili aweze kuunganishwa katika tuhuma hizo na wenzake watano ambao walifikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Kigoma tarehe 31 mwezi Agosti mwaka 2020.
Wakati watuhumiwa hao wanafikishwa Mahakamani, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU alitoa taarifa kwa umma juu ya kutafutwa kwa Madaraka.
Katika hatua nyingine, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoani Mwanza katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi mwaka huu imefanikiwa kuokoa zaidi ya shilingi milioni 87.
Fedha hizo zilirejeshwa wakati wa operesheni ya kufuatilia fedha za umma zilizokuwa zimechepushwa au kufanyiwa ubadhirifu, kinyume na sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.