Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesisitiza kuwa Serikali itaenzi na kuendeleza jitihada, maono na juhudi za Hayati Dkt. John Magufuli hasa katika ulinzi wa rasilimali za Taifa pamoja na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.
Pia, amesema Serikali itaendeleza nidhamu katika matumizi ya fedha za umma, utekelezaji wa miradi ya kimkakati, kuenzi lugha ya Kiswahili, kuwajali wananchi wanyonge na kudumisha umoja wa Kitaifa.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022.
Amesema Serikali itatekeleza kwa kasi miradi ya kimkakati ambayo inalenga kukuza uchumi, kuimarisha huduma za jamii na kuongeza fursa za ajira.
“Kwa kasi tuliyoanza nayo, Serikali itaendelea kuongeza nguvu zake na hatimaye kukamilisha miradi hiyo.” amesema Waziri Mkuu.
Ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na washirika wa maendeleo katika kutekeleza miradi na programu mbalimbali zinazolenga kuimarisha huduma za kiuchumi na kijamii na kuchukua hatua za kukabiliana na majanga mbalimbali yakiwemo magonjwa ya mlipuko kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalam.
Waziri Mkuu Majaliwa ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya shilingi bilioni 116.8 kwa ajili ya Ofisi yake pamoja na taasisi zilizo chini yake kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022.
Amesema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 93.3 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 23.5 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.