Jamii yasisitizwa kuwasaidia watoto yatima

0
222

Jamii imetakiwa kujitolea kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum hasa yatima.

Wito huo umetolewa jijini Dar es salaam na Rais mstaafu wa awamu.ya nne Dkt. Jakaya Kikwete, wakati wa harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwasaidia watoto yatima, iliyoandaliwa na taasisi ya Volunteers In Development.

Dkt. Kikwete amesema suala la kuwasaidia watoto yatima ni la kuuungwa mkono na jamii, pasipo kujali dini na itikadi ya jamii husika.

“Maisha na hali ya watoto yatima yana mitihani na madhila hasa pale wanapoona wamekosa wazazi na walezi wa kuwasaidia, kwani wanakuwa hawana uhakika wa maisha ikiwemo kupata elimu, chakula na malazi, hivyo ni jukumu letu sote kujitoa kwa ajili yao,” amesema Dkt. Kikwete.

Ameongeza kuwa jamii ina wajibu wa kushirikiana katika kuwasaidia watoto yatima ili waweze kufikia ndoto zao kama walivyo watoto wengine.

“Sioni haya kuiomba jamii kuisadia taasisi ya Volunteers In Development ili iweze kutekeleza majukumu yao ya kuwasaidia watoto yatima na wale wenye mahitaji maalum kwa urahisi zaidi,” amesisitiza Rais mstaafu Kikwete.

Ameongeza kuwa mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa Neema na thawabu, hivyo ni vema jamii ikatumia nafasi hiyo kuwasaidia watoto yatima ambao hawajui kesho yao itakuwa vipi.

Aidha, ametoa rai kwa Wafanyabiashara wa bidhaa za chakula kuhakikisha bidhaa muhimu zinazotumika wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani zinapatikana kwa bei nafuu, lengo likiwa ni kuwawezesha wanaofunga kupata bidhaa za kufuturu kwa urahisi.

Kwa upande wake mwakilishi wa taasisi ya Volunteers In Development Dkt. Naima Besta amesema kuwa, ili jamii iendelee kuiamini taasisi hiyo katika kuwasaidia watoto yatima, ni vema wale wote wanaotoa ahadi hadharani wazitimize kwa vitendo.

Katika harambee hiyo, zaidi ya shilingi milioni 60 zimepatikana zikiwa ni fedha taslimu na ahadi kwa ajili ya kuwasaidia watoto yatima, huku lengo likiwa ni kukusanya shilingi milioni 54.