Rekodi ya Simba yavunjwa Misri

0
462

Simba SC imeshindwa kutamba mbele ya miamba ya Misri, Al Ahly, baada ya kukubali kipigo cha goli 1-0 katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Goli hilo pekee la Al Ahly limefungwa na Mohamed Sherif dakika ya 32, na katika msimamo wa Kundi A, inashika nafasi ya pili ikiwa na alama 11, nyuma ya Simba yenye alama 13.

Katika michezo sita ya hatua ya makundi, Simba imeshinda michezo minne, ikitoka sare mmoja na kupoteza mmoja.

Timu zote mbili tayari zilikuwa zimefuzu hatua ya robo fainali ya mashindano hayo makubwa zaidi kwa ngazi ya vilabu barani Afrika kabla ya mchezo wa leo.

Katika mchezo mwingine wa kundi hilo ambao ulikuwa ni wa kukamilisha ratiba, AS Vita ya DR Congo imeibuka na ushindi wa magoli 3-1 dhidi ya Al Merrikh ya Sudan.

Kwa ushindi huo, AS Vita imefikisha alama 7, ikishika nafasi ya tatu, huku Al-Merrikh ikiburuza mkia ikiwa na alama mbili. Timu hizo tayari zilishaondolewa kwenye mashindano hayo.