Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020 imeonyesha kuwepo kwa mashirika ya umma 30 yasiyokuwa na bodi za Wakurugenzi.
Akitoa taarifa kuhusu ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere amesema kuwa kati ya mashirika hayo, 20 hayana bodi kwa muda wa chini ya mwaka mmoja, tisa hayana bodi kwa zaidi ya mwaka mmoja na moja halina bodi kwa miaka miwili.
Amesema mbali na kukosekana kwa bodi katika mashirika hayo ya umma 30, pia mashirika matano yanaongozwa na Kaimu Wakurugenzi wakuu.
CAG Kichere amefafanua kuwa kukosekana kwa bodi kwenye mashirika hayo ya umma kunazorotesha ufanisi wa mashirika hayo na kunasababisha kuchelewa kwa kutolewa maazimio na utekelezaji wa maamuzi muhimu ya kimkakati ikiwa ni pamoja na uidhinishaji wa miongozo, kanuni na sera.
Kufuatia hali hiyo, CAG amependekeza mamlaka za uteuzi zifikirie kuchukua hatua mapema za kuhakikisha zinafanya utambuzi wa bodi ambazo muda wake unakaribia kuisha ili kupata fursa ya kuanza mchakato wa uteuzi mapema lengo likiwa ni kuondoa changamoto hiyo.