Bilioni 1.5 kuwanufaisha wasanii

0
281

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inategemea kutenga kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuendeleza sekta ya sanaa nchini, jitihada zinazolenga kuhakikisha kuwa wasanii wote wananufaika na kazi zao.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa akizungumzia bajeti inayotarajia kuweka na wizara kwenye sanaa, wakati wa uzinduzi wa filamu ya maisha ya Dkt. Magufuli itakayowekwa kwenye Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam.

Akidokeza mambo ambayo wanaendelea kuyasimamia amesema ni pamoja na kuhakikisha Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) inakuwa na manufaa kwa wasanii kwa kuhakikisha kazi zao haziibwi na watu wengine wasiohusika wakanufaika kwazo.

Aidha, amesema wizara hiyo inakusudia kuanzisha tuzo ambazo zitakuwa ni motisha kwa wasanii kufanya kazi bora zaidi.

Ili kupanua vyanzo mbalimbali vinavyoweza kutumika kuiongezea tasnia ya sanaa pesa, Bashungwa amesema hivi sasa wizara yake inashughulikia kurudisha bahati nasibu ya Taifa.

Ametumia nafasi hiyo kuwasihi wasanii kuwa wamoja na watumie muda wao vizuri hapa duniani kuweza kuleta mabadiliko kama aliyofanya Hayati Rais Dkt. John Magufuli.