Wanawake viongozi watakiwa kuchapa kazi

0
233

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Gaudentia Kabaka ametoa rai kwa Wanawake wenye nyadhifa mbalimbali nchini kufanya kazi kwa bidii, kama njia ya kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan na kumuenzi aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. John Mgufuli

Kabaka ametoa rai hiyo jijini Dodoma wakati akitoa salaam za pole za UWT kwa Taifa kufuatia kifo cha Dkt Magufuli na pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Tunampa pole nyingi sana Mama yetu na Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa msiba huu uliotupata wote kwa kumpoteza kiongozi wetu, pia kwa niaba ya UWT kumpongeza sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” amesema Kabaka.

Amesema Wanawake wote walioaminiwa na kupewa uongozi wampe ushirikiano Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya kazi kwa umahiri, kuishi viapo vyao, kuilinda katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwatumikia Watanzania bila ubaguzi.