Maabara bubu hatarini kufungiwa

0
123

Wamiliki wa maabara bubu nchini na ambazo hazina wataalamu wenye vigezo vinavyotakiwa au kuwa na upungufu kulingana na kazi zilizopo wametakiwa kuzisajili na kuwa na watalaamu hadi kufikia Aprili 30, 2021 ili kuepuka kufungiwa.

Agizo hilo limetolewa Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Grace Magembe wakati wa mkutano na Wamiliki wa Maabara binafsi za mkoa wa Dar Es Salaam, mkutano ulio kuwa na kauli mbiu isemayo “Ushirikiano wa Wadau ni nguzo Muhimu katika Utoaji wa Huduma Bora za Afya.”

Dkt. Magembe amesema kumekua na ongezeko kubwa la Maabara bubu nchini ambazo nyingine zinafunguliwa katika makazi ya watu na kuhatarisha maisha ya watu wanaokaa maeneo hayo hususani watoto ambao wana tabia ya kuchezea vitu hatarishi.

“Nimetoa maelekezo kwa mratibu wa maabara mkoa wa Dar Es Salaam kuhakikisha maabara zote ambazo hazijasajiliwa zipewe nafasi ya kusajiliwa hadi kufikia tarehe 30 mwezi Aprili, kinyume na hapo zitafungiwa na wahusika kuchukuliwa hatua kwa kupelekwa kwenye vyombo vya sheria”. Amesema Dkt. Grace.

Pamoja na hayo, Dkt. Magembe amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali za mitaa, vijiji na vitongoji kutoa taarifa kwenye mamlaka husika endapo wataona kuna maabara zimeanzishwa katika maeneo yao ambazo hazijasajiliwa na kulipa ada.