Mabalozi wasisitizwa kutafuta masoko ya bidhaa

0
249

Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali duniani, wameelekezwa kujipanga, kushiriki na kutafuta fursa zitakazowezesha bidhaa mbalimbali za Tanzania kupata masoko ya uhakika katika nchi walizopo.

Maelekezo hayo yametolewa jijini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi wakati akizungumza na mabalozi mbalimbali wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi.

Akitoa maelekezo hayo Waziri Kabudi amesema ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inatamka bayana juu ya Diplomasia ya Uchumi pamoja na kuimarisha sauti ya Tanzania na taswira yake katika medani ya uhusiano wa kikanda na kimataifa. 

Profesa Kabudi amesema ili kufanikisha hilo, balozi zinapaswa kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika jumuiya nyingine za kimataifa zikiwemo Indian Ocean Rim Association, Indian Ocean Tuna Commission, South South Commission na South West Indian Ocean Fisheries Commission.

Amewataka mabalozi hao kuzingatia maelekezo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi aliyoyatoa wakati akizindua Baraza la Wawakilishi ya kutaka Uchumi wa Bluu kupitia uvuvi wa Bahari Kuu unakua na manufaa kwa Wananchi.
 
Aidha, Profesa Kabudi amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) katika maendeleo ya Taifa na kuzielekeza Balozi zianze na ziboreshe kanzi data ya diaspora ikiwa ni pamoja na kuwahimiza kuanzisha Jumuiya zao. 

“Natambua kazi hiyo inaendelea na kwa sasa tuna data za diaspora takribani 98,658 na kuna Jumuiya 77 za diaspora, nichukue fursa hii kusisitiza umuhimu wa Balozi zetu kuboresha na kuharakisha zoezi hili kwa kubuni njia mbalimbali za kuwaandikisha,” amesema Profesa Kabudi.