Rais Samia: Tutatekeleza yote aliyoahidi Dkt. Magufuli

0
271

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa baada ya mazishi ya Dkt. John Magufuli, kinachofuata ni utekelezaji wa ahadi zote ambazo yeye na chama chake (Chama cha Mapinduzi) waliahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Rais Samia amesema hayo wilayani Chato mkoani Geita wakati akitoa salamu za pole kwa familia ya Dkt Magufuli na waombolezaji wengine waliofika kwenye Misa Takatifu ya mazishi ya kiongozi huyo.

Amesema kuwa Tanzania imempoteza Jemedari, lakini watendaji na wasaidizi aliokuwa akifanya nao kazi bado wapo hivyo watatekeleza yale yote aliyoahidi kwa wananchi.

“Tunachokwenda kuzika leo ni kiwiliwili tu, maono yake bado tutaendelea kuyaenzi na kutekeleza,” amesema Rais Samia.

Kuhusu ahadi ya kuifanya wilaya ya Chato kuwa mkoa ambayo Dkt. Magufuli alikuwa ameahidi, Rais Samia amesema kuwa anafahamu kwamba mchakato wa hilo umeanza na amewataka watendaji kuendelea nao, na kwamba wataangalia kama vigezo vimetimia.

Tayari Misa Takatifu ya mazishi ya Dkt Magufuli imemalizika, na sasa mwili unapelekwa nyumbani kwake kwa ajili ya mazishi, ikiwa ni mwisho wa safari yake hapa duniani.