Mufti : Tutamkumbuka Dkt. Magufuli kwa kufanikisha ujenzi wa msikiti

0
192

Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir amesema viongozi wa dini nchini wataendelea kumkumbuka na kumuenzi aliyekuwa Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli, kutokana na ukaribu aliokuwa nao kati yake na viongozi hao.

Mufti ametoa kauli hiyo katika Uwanja wa Magufuli wilayani Chato mkoani Geita,  inapofanyika Misa Takatifu ya Mazishi ya Dkt Magufuli wakati akitoa salamu za Baraza  Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kufuatia kifo cha kiongozi huyo.

Ameongeza kuwa katika shughuli zake mbalimbali hasa uzinduzi wa miradi, Dkt. Magufuli alipenda kuongozana na kuwashirikisha viongozi hao wa dini, ikiwa ni ishara ya kuipa baraka miradi hiyo.

Amesema kwa upande wa waumini wa dini ya kiislamu nchini, watamkumbuka Dkt. Magufuli kwa kuwajengea msikiti mkubwa wa Mfalme Mohammed wa Sita wa Morocco uliopo Makao Makuu ya BAKWATA, Kinondoni mkoani Dar es salaam.

Mufti wa Tanzania amesema mbali na kutoa ombi kwa Mfalme Mohammed wa Sita wa Morocco la kutaka kujengewa msikiti huo, Dkt. Magufuli kila mara alikuwa akifuatilia maendeleo ya ujenzi huo.

Amewataka viongozi wote waliobaki wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kuendeleza miradi yote iliyoasisiwa na Dkt. Magufuli ili ilete manufaa kwa Watanzania.