Kwaheri Shujaa wa Afrika

0
247

Tarehe 17 Machi 2021 ni siku ambayo Watanzania hawataisahau kamwe, na hii ni baada ya wingu jeusi kutanda katika anga la nchi yao kutokana kifo cha Mpambanaji na Jemedari Daktari John Joseph Pombe Magufuli.

Waswahili wana msemo usemao ajuaye siri ya mtungi ni kata!!!

Mungu alifanya kifo ni siri yake na fumbo kubwa kwetu sisi Wanadamu na ndio maana kamchukua Jemedari huyu wakati Watanzania wengi bado wakimhitaji wakisema ni mapema mno kwa yeye kuondoka.

DKt Magufuli umefanya mambo mengi mazuri kwa Taifa lako la Tanzania tena kwa muda mfupi uliowatumikia Watanzania, hakika ulikuwa Mzalendo wa kweli

Tazama rasilimali za Taifa kama vile madini umeyalinda kwa nguvu zako zote na kuyaokoa kutoka midomo ya mbwa mwitu (Mabeberu) walioyachota miaka nenda rudi bila kushiba, lakini sasa wachimbaji wadogo wa Kitanzania wananufaika na rasilimali hiyo

Tazama miundombinu ya barabara, huduma za afya, usafiri wa anga, majini na nchi kavu, hukuiacha nyuma sekta ya elimu, na hapa ndipo Watoto wengi wa Kitanzania hasa kutoka familia zenye kipato cha chini wanafurahia elimu bila malipo.

Yote hayo ni kwa sababu uliamua kuyatoa maisha yako sadaka kwa Watanzania wanyonge kama ulivyosikika ukisema hivyo kwenye hotuba zako mara kwa mara. Hakika Watanzania walipata muda mzuri wa kuwa na wewe.

Wewe Dkt Magufuli hukumuacha nyuma Mola wako, nyakati zote Dunia na Taifa lilipokuwa likipita katika changamoto mbalimbali msisitizo wako ni Tumuombe na Tumtegemee Mungu, mfano wakati wa janga la virusi vys Corona, na kwa sababu hiyo nchi ikavuka salama.

Wewe ni Jemedari hasa, zilipotokea changamoto mbalimbali nchini mwako ulitumia maarifa yako.yote bila kusita kulipigania Taifa lako na kusimama Imara na wale unaowaongoza pasipo kujali dunia inazungumza nini juu yako, na hakika ukafanikiwa kuyashinda mambo mbalimbali.

Uliwapenda sana Wananchi wako, ulipita kila kona ya nchi kujua changamoto zinazowakabili, huku zingine ukizitatua papo kwa papo lakini sasa unapita mule mule ukiwa ndani ya jeneza, huongei tena, ukiwaachia simanzi Watanzania ambao wanajiuliza ni nani atamaliza changamoto zao.

Kwa maneno mafupi nenda Baba, nenda JPM wasalimie watangulizi wako Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Benjamin Mkapa huko walipo na panapo majaliwa tutaonana tena.

Tarehe 19 Machi 2021 nayo itabaki kwenye vitabu vya kumbukumbu baada ya Watanzania kushuhudia Mwana Mama Samia Suluhu Hassan akila kiapo kuwa Rais wa Tanzania na Rais wa kwanza Mwanamke katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Hakika Mungu hujatuacha yatima Watanzania, kwani umemchukua Mfalme John Pombe Joseph Magufuli na kutufuta machozi kwa kutuletea Malkia Samia Suluhu Hassan.

Ni Imani ya Watanzania wengi kuwa Malkia huyu atatuvusha na kutufikisha katika nchi ya mafanikio ambayo Mfalme wetu Dkt Magufuli ulikusudia kutupeleka.

Piga kazi Mama Samia, kamwe usirudi nyuma ili machungu walionayo Watanzania yabaki kuwa historia huku tukisherehekea mazuri aliyotuachia Daktari John Magufuli.