Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam, Jude Thadeus Ruwa’ichi amewataka Watanzania wa dini zote kumcha Mungu kama alivyokuwa akifanya aliyekuwa Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli.
Amesema wakati wa uhai wake Dkt. Magufuli alikuwa mcha Mungu na hilo lilidhihirika kutokana na matendo yake.
Akitoa mahubiri wakati wa Misa Takatifu ya kumuombea Dkt. Magufuli katika Uwanja wa Uhuru mkoani Dar es salaam, Askofu Ruwa’ichi amewataka Watanzania kuendelea kumuombea Kiongozi huyo ambaye alikuwa na mapenzi makubwa na nchi yake.
Amewaomba pia kuendeleza mshikamano, ikiwa ni moja ya njia ya kumuenzi Dkt. Magufuli.
Halikadhalika Askofu Ruwa’ichi amewataka Watanzania kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan, ili aweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa kuwa kazi ya Urais ni jukumu zito.
Ameelezea matumaini yake kuwa Rais Samia ataliongoza Taifa vizuri kutokana na uzoefu alioupata kwa Dkt Magufuli.