Kikwete amlilia Dkt. Magufuli

0
395

Rais mstaafu wa awamu ya nne, Dkt. Jakaya Kikwete ametoa pole kwa Watanzania kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania awamu ya tano, Dkt. John Magufuli kilichotokea Machi 17 mwaka huu.

Kupitia ukurasa wa Twitter, Dkt Kikwete ameandika ujumbe wa simanzi kufuatia kifo hicho, amesema kumpoteza Dkt. Magufuli ni pigo kubwa lisilomithilika kwani ametutoka ghafla bila ya kutazamia.

“Tungetamani John Pombe Joseph Magufuli tuendelee kuwa nawe leo na miaka mingi ijayo, lakini mapenzi ya Mungu hatuna uwezo kuyabadili. Wajibu wetu ni kumuombea kwa mola ampe mapumziko. Daima tutamkumbuka Rais John Pombe Joseph Magufuli kwa mema mengi aliyoifanyia nchi yetu. Hakika Tanzania imepoteza kiongozi mzalendo wa dhati, shupavu, mahiri na makini,” imeeleza taarifa hiyo.

Dkt. Kikwete amesema jambo la faraja kwa Watanzania kwa sasa ni kuwepo kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye hapo awali alikuwa makamu wake kuanzia mwaka 2015 hadi umauti unamkuta.

Pia ametoa pongezi kwa Samia Suluhu Hassan kwa hotuba yake aliyoitoa baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Nampongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa hotuba fupi na nzuri aliyoitoa baada ya kuapishwa na yenye kujenga imani na kuleta matumaini. Tumuombee Rais wetu kwa Mwenyezi Mungu amuongoze vyema kwa kila uamuzi atakaouchukua na kila hatua atakayopiga.”

Dkt. Kikwete ametoa salam za mkono wa pole na rambirambi kwa Mama Janet Magufuli na familia nzima.