Chanjo ya AstraZeneca bado kizungumkuti

0
292

Wataalamu mbalimbali wa masuala ya afya duniani wameelezea kusikitishwa na hali ya taharuki, iliyosababisha baadhi ya nchi kusitisha matumizi ya chanjo ya Corona ya Oxford-AstraZeneca.

Chuo kikuu cha Oxford cha nchini Uingereza kimesema kuwa, bado hakuna takwimu za kutosha za kuwaondoa watu wasiwasi kuwa chanjo hiyo ni salama ama ina madhara.

Nchi za Sweden na Latvia hii leo zimeungana na nchi nyingine za Ulaya kusitisha matumizi ya chanjo hiyo, kufuatia madai kuwa inasababisha kuganda kwa damu.

Ujerumani, Ufaransa, Italia na Hispania zimesema nazo zitasitisha matumizi ya chanjo ya corona ya AstraZeneca.

Nchi nyingine ni Austria ambayo imesitisha kwa muda matumizi ya chanjo hiyo, na Thailand ndiyo ilikuwa ya kwanza barani Asia kusitisha matumizi ya Oxford-AstraZeneca.

Uingereza, Canada na Australia zinaendelea kupeleka chanjo hiyo katika nchi mbalimbali, huku zikiwahakikishia kwamba chanjo hiyo ni salama.

Kwa upande wake Shirika la Afya Duniani (WHO)  pamoja na Taasisi ya Udhibiti wa Dawa Barani Ulaya wamezishauri nchi zote kuendelea na matumizi ya chanjo hiyo ya corona ya  Oxford-AstraZeneca.