Mkoa wa Mbeya kumaliza vifo vya mama na mtoto

0
279

Waziri wa Afya, Dkt. Dorothy Gwajima ameupongeza uongozi wa mkoa wa Mbeya kwa ujenzi wa jengo jipya la huduma ya wazazi katika Hospitali ya Wazazi ya Meta, ujenzi uliofikia 88% kwa miezi 20 kati ya miezi 24 kwa gharama ya bilioni 6.4 kati ya bilioni 9 zinazotarajiwa kukamilisha mradi huo.

Akikagua ujenzi huo Waziri Dkt. Gwajima amesema, “nimefurahishwa sana na ujenzi huu kwa mkoa wa Mbeya haya ni mapinduzi makubwa katika kuendelea huduma za afya ya uzazi na mtoto, nilikwishakupita hapa miaka ya nyuma hali ilikua tete kwenye jengo la zamani. Mkoa mmefanya kazi kubwa na nzuri, jengo linavutia.”

Hospitali hiyo ikikamilika itakuwa na vyumba 223 kwa ajili ya huduma, vyumba vya upasuaji vitatu, vyumba maalumu (VIP ), wodi ya kujifungua pamoja na wodi ya wagonjwa mahututi (ICU), hivyo kumuwezesha kupata huduma zote chini ya uangalizi maalumu.

Hata hivyo Dkt. Gwajima alisema yapo mapinduzi na maboresho makubwa ya ujenzi yaliyofanywa na Serikali nchi nzima katika dhana ya kuendeleza afya ya mama na mtoto kwenye halmashauri kuanzia kwenye zahanati mpaka hospitali za wilaya na mkoa ambapo vituo hivyo vina uwezo wa kufanya upasuaji.

“ Hata kwenye jamii kuna wahudumu wa afya ya jamii wanaofuatilia masuala ya afya ya watoto na wazazi na kutoa ushauri. Serikali kwa kushirikiana na wananchi imejenga zahanati 1198 katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015, vituo vya afya 487 vyenye uwezo wa kufanya upasuaji na vituo vingi vimeanza kutoa huduma hiyo na vile ambavyo bado tunaenda kuviwezesha vianze kutoa huduma hiyo mara moja kwani Serikali imedhamiria kumuokoa mtoto na mwanamke ili waachane na changamoto za kupoteza maisha ya watoto wakiwa tumboni au mwanamke anapojifungua,” amesisitiza.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Mbeya, Albert Chalamila amesema kukamilika kwa jengo hili kutasaidia sana kufuta vifo vya mama na mtoto kwenye mkoa wake kwani jengo hilo litakua na vifaa na vifaa tiba na kuongeza kuwa hadi sasa malalamiko ya akina mama kuhusiana na uzazi yamepungua licha ya ufinyu wa jengo lililopo.

Katika ziara yake mkoani humo Dkt. Gwajima ametembelea pia hospitali ya rufaa ya mkoa Mbeya na kujionea hali ya ujenzi wa jengo la upasuaji lenye vyumba sita vya upasuaji na jengo la dharura na ameahidi wizara itafanya mpango wa ujenzi wa jengo la uzazi kwenye hospitali hiyo ya mkoa ili kuweza kuwapunguzia mzigo hospitali ya wazazi ya meta ambayo ipo chini ya hospitali ya rufaa ya kanda Mbeya.