Mapato yatokanayo na Tanzanite yafikia shilingi bilioni 1.417

0
164

Mapato yatokanayo na Madini ya Tanzanite katika eneo la Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, yameongezeka kutoka shilingi milioni 238 mwaka 2016 na 2017 hadi kufikia shilingi bilioni 1.417 mwaka 2020.

Akiwasilisha taarifa ya eneo tengefu la Mirerani kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila amesema ongezeko la mapato hayo limetokana na kuimarika kwa udhibiti wa madini hayo baada ya kukamilika kwa ujenzi wa ukuta unaozunguka migodi ya Tanzanite mwaka 2018.

Profesa Msanjila ameongeza kuwa ukuta huo umewezesha kupungua kwa matukio ya utoroshaji wa madini yaliyokuwa yakiisababishia Serikali hasara, kuimarisha ulinzi wa watu wanaofanya shughuli mbalimbali na mali zao, kurahisisha shughuli za kiutawala na usimamizi wa rasilimali madini katika eneo hilo na kuzuia utumikishwaji wa watoto katika shughuli za uchimbaji wa madini ya Tanzanite.

Aidha, Profesa Msanjila ameieleza kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa, Kituo cha Pamoja cha Biashara ya Tanzanite kilichojengwa ndani ya ukuta huo sasa kitajulikana kwa jina la Kituo cha Tanzanite cha Magufuli.

Kituo hicho ambacho tayari kinafanya kazi, kinahusisha ofisi mbalimbali zikiwemo zile za Idara ya Uhamiaji, ofisi ya Usalama wa Taifa, ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ofisi ya Jeshi la Polisi, ukumbi wa mikutano na ofisi ya Madini.

Aidha, Profesa Msanjila ameieleza kamati hiyo kuhusu miradi mbalimbali iliyotekelezwa katika eneo hilo la Mirerani ambayo ni pamoja na ujenzi wa barabara ya ndani inayozunguka ukuta, mradi wa ujenzi wa Vyumba viwili vya upekuzi , eneo la kupumzikia na soko la madini.

Akizungumzia manufaa ya kituo cha mfano kwa wachimbaji wadogo cha Katente kilichopo mkoani Geita, Profesa Msanjila amesema kimewezesha kuzalishwa kwa gramu 11. 588.37 za dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo 39.