Serikali yaagiza kuanzishwa minada ya kuuza chai

0
149

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza mkuu wa mkoa wa Njombe,- Mhandisi Marwa Rubirya, kuvichukua hatua viwanda vya chai ambavyo vimekuwa vikinunua majani mabichi ya chai kwa Wakulima na kuwachelewesha malipo yao.
 
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo mkoani Njombe, wakati wa kikao na wadau wa zao la chai.

Amesema viwanda hivyo vimekuwa vikisababisha adha kubwa kwa Wakulima wa chai kwa kuwacheleweshea malipo, baada ya kutaabika kukuza chai yao.

Pia Waziri Mkuu Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo ianzishe minada ya kuuza zao la chai katika ukanda wa maeneo yanayozalisha zao hilo, ili kuwarahisishia Wakulima kupata soko la uhakika na kuacha kutegemea minada ya nje ya nchi.
 
Amesema dhamira ya Serikali ni kuona Wakulima wa zao la chai nchini wananufaika na kilimo hicho, hivyo itaendelea kufuatilia na kuhakikisha hakuna dhuluma yoyote wakati wa manunuzi.

”Lazima wakulima walipwe fedha zao kwa wakati ili waweze kuhudumia mashamba yao na kukidhi mahitaji yao, zao la chai ni miongoni mwa mazao muhimu ya kibiashara yanayoliingizia Taifa fedha za kigeni, huliingiza zaidi ya Dola Milioni 60 za Kimarekani kwa mwaka”, amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
 
Ametumia kikao hicho na wadau wa zao la chai kuwakaribisha Wawekezaji kujenga viwanda vya kuchakata zao la chai nchini kwa kuwa kuna mazingira mazuri ya uwekezaji na malighafi ya kutosha pamoja na nishati ya uhakika.
 
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda amesema suala la ucheleweshwaji wa malipo linalofanywa na baadhi ya wamiliki wa viwanda vya chai halikubaliki, na amewataka Wawekezaji wote wawalipe Wakulima fedha zao kwa wakati.
 
Kuhusu kuwepo kwa minada ya chai nchini, Profesa Mkenda amesema ifikapo mwezi Mei mwaka huu wanatarajia kufungua mnada wa kuuza chai jijini Dar es salaam, hali itakayosaidia kupatikana kwa soko la uhakika.