Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, yaandaa Kongamano la Urithi wa Ukombozi Barani Afrika na kuendelea kukamilisha Mitaala ya vitabu vya masomo ya historia ya Tanzania, ambavyo pamoja na mambo mengine, vitajumuisha mkusanyiko wa historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika na kutoa ufahamu kwa wanafunzi wa jinsi Tanzania ilivyojitoa katika kupigania uhuru wa nchi zingine.
Mpango huo pamoja na kusaidia kuendeleza historia ya nchi, pia utasaidia kutambua na kuenzi tamaduni za Tanzania, pamoja na mchango wa nchi katika kupigania uhuru wa nchi za Barani Afrika.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa Jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu kufanyika kwa kongamano kubwa la kutambua na kuenzi mchango wa historia ya Tanzania, katika ukombozi wa Bara la Afrika, linaloandaliwa na Wizara hiyo kupitia program ya Urithi wa Ukombozi, litakalofanyika Machi 28 mwaka huu, katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere Mkoani Dar es Salaam.
Bashungwa amesema mchango wa Tanzania katika kulikomboa Bara la Afrika haupimiki wala kulinganishwa na thamani yoyote, kutokana na kuhusisha Watanzania kujitoa kwa uhai wao, Mali, vitu, na maarifa kwa ajili ya kuliweka Bara la Afrika kuwa huru na kuwataka Watanzania kujivunia suala hilo.
“Mchango wa Tanzania katika kulikomboa Bara la Afrika haupimiki wala kulinganishwa na thamani yoyote, Watanzania tunapaswa kujivunia Utanzania wetu, nasisitiza haya kwa kuwa vijana wengi wa sasa bado hawajafahamu suala hili, ya kuwa Tanzania wakati wa ukombozi ilikuwa kama Macca au Jelusalemu ya Afrika, mchango wetu umetambulika duniani kote” amesema Bashungwa.
Amesema kutokana na mchango huo wa Tanzania kwa Afrika, Mwaka 1963 Umoja wa Nchi za Afrika Afrika uliekeleza Tanzania kuwa Makao Makuu ya Kamati ya Ukombozi ya Afrika hadi nchi ya Afrika Kusini ilipopata Uhuru Mwaka 1994 mwaka ambao Nchi zote za Afrika zilikombolewa.