Serikali imeanza maandalizi ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha Mwanza-Isaka yenye urefu wa kilomita 341, ambayo itajengwa kwa gharama ya shilingi trilioni 3.0267 ambazo ni fedha za ndani.
Katika mradi huo bandari kavu na stesheni vinatarajiwa kujengwa katika eneo la Malampaka wilayani Maswa mkoani Simiyu.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amebainisha hayo katika kikao cha pamoja cha wadau, kilichofanyika wilayani Maswa mkoani Simiyu kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja juu ya utekelezaji wa mradi huo.
“Hapa Malampaka tutakuwa na kambi ya watu zaidi ya 3000 kwa hiyo ni vizuri wananchi wakaandaliwa ili waweze kushiriki fursa mbalimbali, tunatarajia pia kujenga bandari kavu kama ilivyo Isaka, mizigo kutoka mikoa mbalimbali itaishia hapa Malampaka, pia tutajenga stesheni kubwa yenye mita za mraba 8,000 ambayo ndani itakuwa na benki, maduka na huduma nyingine,” amesema Kadogosa.
Aidha, Kadogosa ametoa wito kwa wananchi na wadau wengine kutoka taasisi mbalimbali kushirikiana na TRC ili utekelezaji wa mradi huo usiathiri shughuli mbalimbali za wananchi huku akiahidi shirika hilo kuendelea kusimamia upatikanaji wa fursa kwa usawa kama ilivyoelekezwa na Rais Dkt John Magufuli.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka katika kikao hicho amesema mkoa wa Simiyu umepokea mradi huo kwa asilimia 100 na kuahidi kutoa ushirikiano, huku akiwahakikishia usalama wakandarasi na watu wote watakaohusika na utekelezaji wa mradi huo.