Masharti 12 ya TCRA kwa kampuni za simu kuhusu vifurushi

0
250

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa masharti au vigezo ambavyo kampuni za huduma ya mawasiliano nchini zinatakiwa kufuata ikiwa ni njia ya kuboresha huduma za mawasiliano.

Uamuzi huo umekuja baada ya mamlaka hiyo kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu uboreshwaji wa vifurushi kufuatia kuwepo malalamiko ya gharama kubwa na wizi wa vifurushi vyao.

Masharti yaliyotolewa na TCRA ambayo yametokana na kutungwa kwa kanuni ndogo za mawasiliano ni;

  1. Mtoa huduma hatatoa huduma za vifurushi bila kibali cha mamlaka;
  2. Mtoa huduma atahakikisha kwamba bei za vifurushi zinazingatia bei husika ya chini na ya juu zilizowekwa na mamlaka;
  3. Mtoa huduma atatumia lugha rahisi na vigezo na masharti yaliyo wazi kuhusu vifurushi vinavyotolewa;
  4. Vifurushi vinavyotolewa kwa mtumiaji havitaondolewa, havitarekebishwa au kubadilishwa ndani ya miezi mitatu baada ya kuidhinishwa;
  5. Mtoa huduma atatoa fursa kwa mtumiaji wa huduma za mawasiliano kuchagua na kujiunga na vifurushi visivyokuwa na ukomo wa muda wa matumizi vitakavyopatikana kwenye menyu kuu na vitatumia jina linalofanana kwa vifurushi hivyo ili vitambulike kwa wepesi;
  6. Mtoa huduma atatoa taarifa kila wakati matumizi ya kifurushi yatakapofikia asilimia 75 na 100 kwa vifurushi vya muda wa maongezi, data na SMS;
  7. Mtoa huduma ataweka programu rununu (Mobile App) ya kumwezesha mtumiaji wa huduma mwenye simu janja kufuatilia matumizi yake ya data kwa kupakua programu rununu hiyo ya mtoa huduma;
  8. Mtoa huduma ataweka utaratibu unaomuwezesha anayejiunga na huduma za vifurushi kuchagua na kukubali kutozwa gharama zisizokuwa kwenye vifurushi mara muda wa vifurushi alivyojiunga nacho au uniti za kifurushi husika kumalizika.Utaratibu huu wa kuchagua na kukubali utakuwa chaguo msingi mpaka pale anayejiunga achague na kukubali kutumia gharama nje ya kifurushi;
  9. Mtoa huduma ataweka utaratibu wa kumwezesha aliyejiunga na kifurushi chochote kuendelea kutumia muda wa uniti za kifurushi ambazo zitakuwa zimesalia ndani ya muda wa matumizi uliowekwa kwa kununua tena kifurushi hicho hicho kabla ya kumalizika kwa muda wake;
  10. Mtoa huduma ataweka utaratibu au mfumo wa kumwezesha mtumiaji wa huduma kuhamisha uniti za kifurushi kwenda kwa mtumiaji mwingine wa ndani ya mtandao wake kwa sharti kwamba:
    (a) Kiasi cha chini cha kuhamisha kitakuwa ni 250MB, na mtumiaji anaweza kuwahamishia watumiaji wasiozidi wawili; na
    (b) Mtumiaji aliyehamishiwa uniti za kifurushi hataruhusiwa kumhamishia mtumiaji mwingine uniti hizo au sehemu ya uniti alizohamishiwa;
  11. Mtoa huduma hatoruhusiwa kupunguza kasi ya data kwenye kifurushi cha mteja ndani ya muda wa kifurushi husika;
  12. Mtoa huduma hatofanya promosheni zaidi ya tatu au kutoa ofa maalum zaidi ya tatu kwa wakati mmoja kupitia huduma za sauti, SMS na data.

Mamlaka hiyo imesema utekelezaji wa kanuni ndogo hizi utaanza rasmi Aprili 2, 2021, na kwamba wataendelea kushughulikia mambo mengi zaidi yanayolalamikiwa na watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini.