Rais Magufuli ampa waziri siku saba polisi wastaafu walipwe mafao yao

0
260

Rais Dkt. Magufuli ametoa wiki moja kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene kuhakikisha kuwa askari wote wastaafu wanalipwa mafao yao.

Dkt. Magufuli ametoa agizo hilo leo akizungumza na askari polisi pamoja na wananchi katika viwanja vya Makao Makuu ya Jeshi la Polisi eneo la Kurasini, Dar es Salaam, muda mfupi baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda cha kushona sare za jeshi hilo na kuzindua majengo ya ofisi, madarasa na mabweni ya Chuo cha Taaluma ya Polisi.

Ameeleza kutofurahishwa na wasaidizi wake kutotekeleza majukumu yao na mara nyingi wakisubiri hadi Rais afike atoe maelekezo.

“Hili ni tatizo la wakubwa wenu wizarani… hawawezi wastaafu wa polisi wakamsubiri hadi Rais ndiye akashughulike nao,” amesema Rais Dkt. Magufuli huku akiwataka watendaji kutimiza majukumu yao.

Katika hatua nyingine amekataa ombi la Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ambayo imeiomba serikali kuu iisaidie kulipa deni la bilioni 12.195 ambalo inadaiwa na Benki ya CRDB.

Akitoa ombi hilo, Mbunge wa Temeke, Dorothy Kilave ameiomba serikali ilipe fedha hizo ambazo ilipoka kwa ajili ya kulipa fidia wananchi walioondolewa kwenye maeneo yao kupisha mradi wa DMDP.

“Ninyi manispaa mmekaa, mkaenda kuzungumza na CRDB, mazungumzo yale wala hayajulikani mlikuwa mnazungumza nini… Mmeshindwa kulipa mnataka serikali ilipe hilo deni… Hilo msahau, ninyi mtalibeba wenyewe,” amesisitiza Dkt. Magufuli

Akiwa katika jambo hilo amesema kitendo cha manispaa hiyo kukopa fedha kutoka benki ya kibiashara na kulipa kwa riba ni matumizi mabaya ya fedha za umma.