Klabu ya soka ya Namungo Fc ya Tanzania imefanikiwa kutinga hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika Licha ya Kupoteza mchezo wa Mkondo wa pili wa hatua ya tatu ya michuano hiyo dhidi ya CD De Agosto.
Namungo imekubali kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa miamba hiyo ya Angola na kufanikiwa kusonga mbele kwa uwiano wa Mabao 7-5 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 6-2 katika mchezo wa Mkondo wa kwanza dhidi ya CD De Agosto.
Hii ni mara ya kwanza kwa Namungo maarufu kama wauaji wa kusini kushiriki Michuano hiyo ya Kimataifa na kufanikiwa kutinga hatua ya Makundi ya kombe la shirikisho.
Namungo walianza kampeni ya michuano hiyo kwa kuibanjua Al Rabita ya Sudan Kusini na kisha kuiondosha mashindanoni Al Hilal Obeid ya Sudan na sasa imeiondosha CD de Agosto ya Angola.
Kutokana na matokeo hayo, Namungo inatinga hatua ya makundi na tayari imepangwa Kundi D sambamba na Raja Casablanca ya Morocco, Pyramids FC ya Misri na Nkana FC ya Zambia.