Wananchi watakiwa kutosubiri matamko kujikinga na magonjwa

0
205

Serikali imewataka viongozi wa serikali, sekta binafsi, viongozi wa kijamii na wananchi kwa ujumla kuacha kusubiri matamko zaidi bali waamke na kuwajibika katika nafasi zao katika kutoa elimu kwa wananchi juu ya kujikinga na magonjwa mbalimbali ya mlipuko katika maeneo yao.

Waziri wa Afya, Dkt. Dorothy Gwajima amesema hayo wakati akitoa tamko la serikali lenye lengo la kuongeza kasi katika kuchukua tahadhari kujikinga na magonjwa ya mlipuko na magonjwa katika mfumo wa hewa.

“Mheshimiwa Rais na Waziri Mkuu wameshafanya kazi kubwa na nzuri ya kutoa matamko ya kukumbusha na kuelimisha taifa juu ya mwelekeo wa tahadhari za kuchukua ili kuepuka mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19. Vilevile, viongozi wa wizara ya afya tumetoa matamko mbalimbali ya kuwakumbusha na kuwaelimisha wananchi kuchukua tahadhari,” amesema Dkt. Gwajima.

Dkt Gwajima amesema jukumu la kinga dhidi ya magonjwa yote yakiwemo ya kuambukiza na yasiyoambukiza ni la kila mtu katika nafasi yake kuhakikisha wanachukua tahadhari kujikinga na magonjwa hayo.

Amebainisha kuwa kila mwaka katika kipindi cha Novemba hadi Machi wimbi la magonjwa yanayoathiri mifumo ya upumuaji na chakula huongezeka kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa huku ikiwatoa wasiwasi wananchi kuendelea kuchukua tahadhari.

Amesema magonjwa hayo yanaweza kusababishwa na vimelea vya bakteria, virusi na fangasi huambukiza kutoka kwa mtu mmoja kwenda mwingine kwa njia mbalimbali ikiwemo hewa, kula au kunywa kitu ambacho siyo kisafi na salama.

Wananchi wametakiwa kuondoa hofu zinazojengwa kwa sababu hofu inaleta madhara zaidi kiafya. “Vifo vingi vinavyotokea duniani asilimia 90 hutokea kwasababu watu wanatanguliza hofu zaidi,”amesema

Aidha Dkt Gwajima amewataka wananchi kuendeleza tabia ya kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi tiririka na sabuni, iwapo maji tiririka na sabuni hakuna, wanatakiwa kutumia vipukusi (sanitizer), kuvaa barakoa kwa kuzingatia muongozo uliotolewa na wizara hususani katika maeneo ya msongamano.

“Naelekeza wataalamu wa lishe ngazi zote kuandaa daftari la orodha ya vyakula vya asili vinavyopatikana eneo husika na kutoa elimu ya milo ipi iandaliwe kama kielelezo cha lishe bora, tuache kuamini kuwa lishe bora ni vyakula vya kisasa vya biashara na vya bei ghali,” amesema.