JPM atoa sharti jina lake kutumiwa Stendi ya Mbezi Luis

0
411

Rais wa Tanzania, Dkt. John amezindua Stendi ya kimataifa ya mabasi yanayokwenda mikoani na nje ya nchi, ambapo amekubali ombi la Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Selemani Jafo la kuiita stendi hiyo, Stendi Kuu ya Magufuli.

Akijibu ombi hilo la waziri wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye hafla hiyo, Rais Magufuli amemwambia Waziri Jafo amejichongea mwenyewe kutumiaji jina lake (Rais), kwani hatakubali wananchi wa chini wanaotumia eneo hilo wanyanyasike.

Amesema kumekuwepo na utamaduni ambao baada ya miradi mbalimbali kukamilika, wamachinga, mama ntilie na wafanyabiashara wengine wadogo huondolewa kwenye maeneo yao.

Kutokana na stendi hiyo kuitwa jina lake, na kwa kuwa yeye ni muwakilishi wa wanyonge, basi hataki kuona mfanyabishara yeyote mwenye kitambulisho cha mjasiriamali au dereva bodaboda anafukuzwa kutoka kwenye stendi hiyo.

Hata hivyo, amewasihi wote watakaotumia mradi huo kuhakikisha wanautunza na kwamba asingependa kuona anafika hapo siku nyingine anakuta kuta zimechorwa chorwa.

Ujenzi wa mradi huo umegharimu jumla ya shilingi bilioni 50.9 ikiwa ni pamoja na daraja. Utachukua mabasi 3,456 na kutakuwa na maegesho ya magari juu na chini.

Mradi huo ambao unaanza kutumika Februari 25, 2021 umetoa ajira 600 katika kipindi cha ujenzi.

Aidha, unatarajiwa kutoa ajira 10,000 utakapoanza kutumika na kuwezesha ukusanyaji mapato ya shilingi bilioni 10 kwa mwaka.