Mbunge ataka kuanzishwa divisheni ya familia kwenye mahakama

0
402

Serikali imeshauriwa kuanzisha divisheni ya familia ambayo itashughulika mashauri ya ndoa, talaka na mirathi ili kuwaondolewa wananchi adha wanayopata kwa mashauri yao kuchelewa katika mfumo wa kawaida wa mahakama.

Rai hiyo imetolewa bungeni mjini Dodoma na Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Kigoma, Zainab Katimba wakati akiuliza swali la nyongeza lililotokana na swali la msingi lililohoji mpango wa serikali wa kubadili sheria kandamizi, ili ziendane na wakati.

Bi. Katimba amehoji, kama ambavyo serikali ilivyoanzisha mahakama ya rushwa na mahakama ya ardhi, je haioni kuna umuhimu wa kuwa na mahakama ya familia, kwani kucheleweshwa kwa mashauri ya familia kwenye mfumo wa kawaida wa mahakama ni sawa na kuwanyima wahusika haki yao.

Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geofrey Pinda amesema ushauri huo ni mzuri sana na kwamba ataufikisha katika mamlaka mbalimbali zinazohusika ili uweze kufanyiwa kazi.

“… sheria zote zinatungwa hapa bungeni. Tusema tu tumepokea wazo lake na tutalipitisha katika mamlaka mbalimbali za kuangalia zile modality [taratibu] za kuanzisha chombo kama hiki ili tuweze kufikia maamuzi halisi,” amesema Pinda.

Awali akitoa majibu ya swali la msingi amesema kuwa serikali haina sheria kandamizi kwani sheria zote hutungwa na bunge ambalo halijawahi kutunga sheria kandaimizi.

“Serikali inaendelea na hatua mbalimbali za kupitia sheria za usimamizi wa mirathi na sheria za kimila,” ameongeza Pinda huku akitanabaisha kuwa miongoni mwa mabadiliko ambayo wizara hiyo inaendelea nayo ni kutafsiri sheria kwa lugha ya Kiswahili na kuweka vifungu vitakavyotaka hukumu zitolewe kwa Kiswahili ili kuongeza tija.